Sunnah katika Swalah ya Kusuwf (Kupatwa kwa Jua /Mwezi
YALIYOSUNIWA KWA MWENYE KUSHUHUDIA KUSUWF (KUPATWA KWA JUA /MWEZI
1- Akithirishe dhikri, kuomba maghfirah, kupiga takbiyr, kutoa swadaqah na amali nyingine njema.
‘Aaishah anasema kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: ((Mtakapoona hilo, basi mwombeni Allaah, pigeni takbiyr, swalini na toeni swadaqah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1044) na Muslim ( 901)].
Na Asmaa anasema: “Hakika Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniamuru nimwache huru mtumwa jua lilipopatwa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1056) na Muslim (903)].
2- Aende kuswali kwa Jamaa Msikitini
Hadiyth ya ‘Aaishah inaeleza: “Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipanda asubuhi kipando (mnyama), jua likapatwa, akarejea dhuhaa. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akapita baina ya vyumba, kisha akasimama na kuswali”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1056) na Muslim ( 903)].
‘Aaishah anasema tena kwenye tamshi lililopokelewa na Muslim: “Nikatoka na wanawake katikati ya vyumba. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaja akiwa ameshuka toka juu ya kipando chake mpaka akafika sehemu yake aliyokuwa anaswalia”.
Al-Haafidh anasema kwenye Al Fat-h (3/633): “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ndani ya kipando hicho kutokana na kifo cha mwanawe Ibraahiym. Aliporejea, alikwenda Msikitini na hakuswali nje uwanjani. Na Sunnah katika Swalaah ya Kupatwa Jua ni kuswaliwa Msikitini, na lau si hivyo, kuswalia kwake jangwani kungelikuwa ni bora zaidi kwa kuwa ni wepesi kuona jua likiachiliwa. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.
3- Wanawake watoke kwenda kuswali
Ni kutokana na Hadiyth ya Asmaa binti Abiy Bakri aliyesema: “Nilimwendea ‘Aaishah mke wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) jua lilipopatwa. Nikawakuta watu wamesimama wanaswali, naye pia kasimama anaswali”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1053) na Muslim ( 905)].
Tumeshalieleza tamko la ‘Aaishah aliposema: “Nikatoka pamoja na wanawake katikati ya vyumba Msikitini.”
Mwanamke mwenye kuchelea fitna husameheka kwenda Msikitini, na badala yake ataswalia nyumbani peke yake.
4- Ainadie Swalaah kwa kusema “As-Swalaatu Jaami’ah” bila adhana wala iqaamah
Imepokelewa toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amri (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema:”Jua lilipopatwa wakati wa enzi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) palinadiwa: "As-Swalaatu Jaami’ah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1045)].
Swalaah hii haina adhana wala iqaamah kwa makubaliano ya Maulamaa wote.
5- Khutbah baada ya Swalaah
Katika Swalaah hii, imesuniwa kutolewa khutbah kama khutbah ya Swalaah ya ‘Iyd kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema kwamba baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumaliza Swalaah, alisimama na kuwakhutubia watu. Alimhimidi Allaah na kumsifu, kisha akasema: ((Hakika jua na mwezi ni alama mbili kati ya Alama za Allaah ‘Azza wa Jalla. Havipatwi kwa kufa mtu wala kwa kuzaliwa, na mnapoona vimepatwa, basi mwombeni Allaah, tamkeni takbiyr, swalini na toeni swadaqah)). [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja nyuma kidogo].
Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy, Is-Haaq na Maulamaa wengi wa Hadiyth. [Al-Majmu’u (5/52), Asnaa Al-Matwaalib (1/286), Fat-hul Baariy (2/620) na Bidaayatul Mujtahid (1/311)]
Abu Haniyfah, Maalik na Ahmadwamesema kwamba Swalaah ya Kusuwf haina khutbah!! [Al-Badaai-’i (1/282), Mawaahibul Jaliyl (2/202), Al-Mughniy (2/425) na rejea zilizotangulia]
Wengine wamesema kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakukusudia khasa khutbah kwa vipengele vyake katika Swalaah hiyo, bali alikuwa anataka kuwabainishia watu jibu kwa wale wenye kuitakidi kwamba kupatwa jua kunatokana na kifo cha baadhi ya watu.
Haya yanajibiwa na yaliyomo kwenye Hadiyth Swahiyh zinazoelezea kwa uwazi kuhusu khutbah, masharti yake, himdi, kumsifu Allaah, mawaidha na mengineyo yanayobainishwa humo. Khutbah haihusiani na kuwajulisha tu watu sababu ya kusuwf, bali asili ya mambo ni kumfuata Nabiy, na mambo yanayomuhusu yeye pekee pasina wengine hayathibiti ila kwa dalili. [Fat-hul Baariy cha Ibn Hajar (2/620) chapa ya As-Salafiyyah]
Inaendelea.....
Na Allaah anajua
Maoni
Chapisha Maoni