Namna ya Kuswali Swalat Kusuwf (Swalah ya Kupatwa kwa Jua/Mwezi

 NAMNA YA KUSWALI SWALAH YA KUPATWA KWA JUA/MWEZI 


Swalaah ya Kusuwf ni rakaa mbili tu, hakuna mabishano kati ya Maulamaa kuhusu hili. Walilobishania ni utendaji wake kwa kauli tofauti. Zilizo mashuhuri zaidi ni mbili:

 

Ya kwanza:

 

Ni rakaa mbili. Kila rakaa ina visimamo viwili, visomo viwili, rukuu mbili na sijdah mbili. Wanaosema haya ni Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad. [Ad-Dusuwqiy (1/405), Al-Ummu (1/215), Kash-Shaaful Qinaa (2/62) na Al-Mughniy (2/422)]

 

Dalili zao ni:

 

1- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema: “Jua lilipatwa wakati wa enzi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Nabiy akaswali pamoja na watu. Akasimama kisimamo kirefu cha kiasi cha kusoma Suwrat Al-Baqarah. Kisha alirukuu rukuu ndefu, halafu akasimama kisimamo kirefu chini kidogo ya kisimamo cha kwanza. Kisha alirukuu rukuu ndefu chini kidogo ya rukuu ya kwanza”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1046) na Muslim (901)].

 

2- Hadiyth ya ‘Aaishah isemayo kwamba Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali siku jua lilipopatwa. Alisimama akapiga takbiyr, akasoma kisomo kirefu, kisha alirukuu rukuu ndefu. Halafu alinyanyua kichwa chake akasema: Sami’a Allaahu liman hamidah, na akasimama tena kama alivyokuwa. Kisha alisoma kisomo kirefu chini ya kisomo cha mwanzo, halafu alirukuu rukuu ndefu chini ya rukuu ya kwanza, kisha akasujudu sijdah ndefu, halafu akafanya katika rakaa ya mwisho mfano wa hivyo, kisha akatoa tasliym”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1047) na Muslim (901)].

 

3- Hadiyth ya Jaabir aliyesema: “Jua lilipatwa enzi ya Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika siku ya joto kali mno. Akawaswalisha Maswahaba wake na akakirefusha kisomo mpaka wakaanza kuanguka. Kisha alirukuu akarefusha, halafu akanyanyuka akarefusha, kisha akarukuu na kurefusha, halafu akasujudu sijdah mbili, kisha akasimama na kufanya mfano wa hayo. Zilikuwa ni rakaa nne na sijdah nne”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (904), Abu Daawuud (1179), An-Nasaaiy (1/217) na Ahmad (3/374)].

 

 Ya pili:

 

Ni rakaa mbili. Kila rakaa ina kisimamo kimoja, rukuu moja na sijdah mbili kama Sunnah nyinginezo. Anayesema hivi ni Abu Haniyfah. Ibn Hazm amekhiyarisha kati ya namna zote. [Al-Badaai-’i (1/281), Tabyiynul Haqaaiq (1/228), Al-Muhalla (5/95) na Bidaayatul Mujtahid (1/307)]

 

Hoja za Abu Haniyfah na wenye kukubaliana naye ni:

 

Hadiyth ya Abu Bakrah aliyesema: “Jua lilipatwa enzi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akatoka akiliburura joho lake hadi akaishilia Msikitini. Watu wakamwendea haraka, akaswali nao rakaa mbili”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1063), An-Nasaaiy (3/146) na At-Twayaalsaa (716)].

 

Wamesema: ”Swalaah yoyote, ni Swalaah iliyozoeleka”. Na katika riwaya ya An-Nasaaiy: “Akaswali rakaa mbili kama wanavyoswali”.

 

2- Hadiyth ya An Nu’umaan bin Bashiyr aliyesema: “Jua lilipatwa enzi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akaanza kuswali rakaa mbili mbili huku akiomba mpaka likaachiliwa”. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1193), Ahmad (4/267) na At-Twahaawiy. Angalia Al-Irwaa (3/131)].

 

Ibn Hazm kasema: “Tamshi hili (yaani kukariri rakaa mbili) linawajibisha tuliyoyaeleza”.

 

Inaendelea.....


Na Allaah anajua zaidi 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Eda: Maana ya Eda, Hikma ya Eda , Hukmu zake, Mambo yanayopasa na uyasiyopasa kwa mwenye Eda

Ramadhwaan ni Mwezi wa Du’aa na Du’aa hutakabaliwa