Maswali Mchanganyiko kuhusu Swalah ya Kusuwf (Swalah ya Kupatwa kwa Jua/Mwezi

 Je, Husomwa Hwa Sauti Au Kimya Kimya?

 

Ahmad, Is-Haaq na Maswahibu wawili wa Abu Haniyfah wanasema kwamba ni Sunnah kusoma kwa sauti kinyume na Jamhuri. [Rejea zilizotangulia kuhusiana na namna ya kuswali]

Dalili zao ni:

 

1- Hadiyth ya ‘Aaishah asemaye: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma kwa sauti katika Swalaah ya Khusuwf. Anapomaliza kusoma, hupiga takbiyr akarukuu, na anaponyanyuka toka kwenye rukuu husema: “Sami’a Allaahu liman hamidahu, Rabbanaa walakal Hamdu”. Kisha hufanya tena kisomo katika Swalaah ya Kusuwf rukuu nne katika rakaa mbili na sijdah nne”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1065)].

 

2- Ni Naafilah iliyoruhusiwa kuswaliwa kwa jamaa. Hivyo basi, sehemu ya Sunnah yake ni kusomwa kwa sauti kama ilivyo kwa Swalaah za ‘Iyd, Tarawehe na Kuomba Mvua.

 

Jamhuri wamesema: “Husomwa kwa sauti katika Swalaah ya Kupatwa Mwezi tu, ama Kupatwa Jua haisomwi kwa sauti”. Hoja yao ni:

 

1- Yaliyomo kwenye Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas iliyotangulia isemayo: “Akasimama kisimamo kirefu cha kiasi cha kusoma Suwrat Al-Baqarah”. Lakini hili haliwajibishi kuwa hakusoma kwa sauti bali inawezekana kuwa alisikia kutoka kwake Suwrah kadhaa alizozikadiria urefu wake na Al-Baqarah, au  alikuwepo sehemu ambayo sauti haikuwa ikimfikia.

 

2- Yaliyosimuliwa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Nilikisia kisomo cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).“ [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1187) na Al-Bayhaqiy (3/338)].

 

Wamesema: “Lau angelisoma kwa sauti, pasingehitajika dhana au makisio”. Nao wamejibiwa kwamba kauli hiyo haijathibiti kwa ‘Aaishah, kisha inapingana na kauli yake sahihi inayothibitisha Nabiy kusoma kwa sauti.

 

3- Hadiyth ya Samurah bin Jun-dub akisema: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Swalaah ya Kupatwa Jua, nami sikuisikia sauti yake”. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (562), Abu Daawuud (1184), An-Nasaaiy (5/19) na Ibn Maajah (1264)]

 

Hili linajibiwa kwa Hadiyth iliyotangulia ya Ibn ‘Abbaas. Hadiyth Swahiyh haiwezi kurejeshwa kwa ajili ya Hadiyth hii. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

· Je, Mbali Na Swalaah Ya Kusuwf, Panaweza Kuswaliwa Pakitokea Matukio Ya Kuonyesha Nguvu Za Allaah Kama Matetemeko Na Mengineyo?

 

Maulamaa wana kauli nne kuhusiana na suala hili:

 

Ya kwanza:

 

Imesuniwa kuswali kwa kila janga au tukio la kuogofya kama tetemeko, upepo mkali, radi na mfano wa hayo. Ni kauli ya Abu Haniyfah, Ibn Hazm na riwaya toka kwa Ahmad.

 

Ya pili:

 

Haiswaliwi Swalaah yoyote kutokana na matukio isipokuwa Kupatwa Jua na Mwezi tu. Hii ni kauli ya Maalik.

 

Ya tatu: Haiswaliwi Swalaah yoyote kutokana na matukio isipokuwa Kupatwa Jua na Mwezi na tetemeko la kudumu. Ni kauli ya Hanbali.

 

Ya nne: Haiswaliwi kwa jamaa isipokuwa Swalaah ya Kupatwa Jua na Mwezi, na kama kuna tukio jingine, basi mtu akae kwake nyumbani aswali na aombe. Ni kauli ya Ash-Shaafi’iy.

 

Ninasema: “Huenda kauli hii ndio iliyo karibu zaidi na usahihi. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.”


Na Allaah anajua zaidi 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Eda: Maana ya Eda, Hikma ya Eda , Hukmu zake, Mambo yanayopasa na uyasiyopasa kwa mwenye Eda

Namna ya Kuswali Swalat Kusuwf (Swalah ya Kupatwa kwa Jua/Mwezi

Ramadhwaan ni Mwezi wa Du’aa na Du’aa hutakabaliwa