Watu Wanaowajibika Kutoa Zakaah
WANAOWAJIBIKA KUTOA ZAKAAH
- Muislam anayemiliki Niswaab, nacho ni 'Kiwango maalum cha mali’ kilichowekwa na shariy’ah katika aina yoyote ile ya mali inayowajibika kuitolea Zakaah.
- Niswaab hiyo lazima iwe ishatolewa ndani yake mahitajio ya dharura ya lazima kama vile chakula, mavazi, makazi, vyombo vya nyumbani, chombo cha usafiri na vyombo vyake vya kufanyia kazi, madeni n.k.
- Lazima kiwango hicho kiwe kimemilikiwa kwa muda wa mwaka mzima (mwaka wa Kiislam) bila kupungua katika wakati wowote ule ndani ya mwaka huo, na kama kitapungua katika wakati wowote ule kabla ya kutimia mwaka, basi hesabu nyingine mpya itaanzwa kuanzia pale kinapokamilika tena Kiwango hicho.
Amesema Imaam An-Nawawiy:
"Madhehebu yetu na madhehebu ya Imaam Malik na Ahmad na ya ‘ulamaa walio wengi ni kuwa; Mali inayotolewa Zakaah kwa ajili yake, kama vile dhahabu, fedha na wanyama wa kufugwa, lazima kiwango chake kibaki kwa muda wa mwaka mzima bila kupungua. Na wakati wowote ule kitakapopungua, basi mwaka wake unakatika, na wakati wowote ule kitakapotimia tena, unaanza kuhesabiwa mwaka mwingine".
Ama Abuu Haniyfah anasema:
"Kinachotakiwa ni kuwepo kwa Kiwango (Niswaab) mwanzo wa mwaka na mwisho wake, na haidhuru iwapo kitapungua katikati ya mwaka, hata kama mtu alikuwa nazo Dirham mia mbili kisha zikapotea zote katikati ya mwaka na akabakiwa na dhirham moja tu, au kama alikuwa na kondoo arubaini wakapungua na akabaki mmoja tu, kisha mwisho wa mwaka akaweza kumiliki (Dirham) mia mbili kamili au (kondoo) arubaini kamili, basi itawajibika Zakaah kwa vyote".
Masharti haya hayahusiani na Zakaah za mazao na matunda, kwa sababu vitu hivyo Zakaah yake inatolewa siku ya mavuno.
Allaah Anasema:
وَآتُواْ حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ
"Na toeni haki yake (Zakaah) siku ya kuvunwa kwake". [Al-An’aam: 141]
MTOTO NA MTU MWENYE UPUNGUFU WA AKILI
Inamuwajibikia aliyekabidhiwa mali ya yatima au ya mtu mwenye upungufu wa akili kuitolea Zakaah mali hiyo ikifikia kiwango chake.
Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru (Radhwiya Allaahu ‘anhu), anasema kuwa; Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Mwenye kumlea yatima mwenye mali, basi aifanyie biashara mali hiyo na asiiache mpaka ikamalizika kwa kuliwa na Swadaqah (Zakaah)".
Anasema Shaykh Sayyid Saabiq katika Fiqhis Sunnah kuwa; Isnadi yake ina udhaifu ndani yake. Akaendelea kusema:
“Anasema Al-Haafidh kuwa Hadiyth hii ina ushahidi kuwa ni 'Mursal' iliyorushwa moja kwa moja mpaka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bila ya kutaja isnadi. Ama Imaam Ash-Shaafi’iy ameikubali (hadithi hii) kwa sababu zipo Hadiyth nyingi zinazoelezea juu ya kuwajibika kwa Zakaah katika mali yoyote ile. Anasema Imaam At-Tirmidhiy kuwa wanavyuoni wamekhitalifiana juu ya kuwajibika kuitolea Zakaah mali ya yatima,” amemaliza kusema Shaykh Sayyid Saabiq.
MTU MWENYE DENI
Mwenye kumiliki kiwango kinachomwajibisha kutoka Zakaah, na wakati huo huo anadaiwa, kwanza anatoa kiasi cha deni analodaiwa, kisha anailipia Zakaah mali iliyobaki ikiwa bado inafikia kiwango cha kutolewa Zakaah. Ama ikiwa mali iliyobaki haifikii kiwango, basi hatoi Zakaah, kwa sababu wakati huo anahesabiwa kuwa ni mtu fakiri, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"Hatoi Swadaqah (Zakaah) isipokuwa mtu tajiri". [Ahmad]
Na amesema:
"Ichukuliwa (mali ya Zakaah) kutoka kwa matajiri wao na kurudishiwa mafakiri wao".
MTU ALIYEFARIKI
Anasema Sayyid Saabiq katika Fiqhis Sunnah kuwa, katika madhehebu ya Maimaam Ash-Shaafi’iy na Ahmad na Abuu Thawr, ni kuwa mtu akifarki na akaacha deni la Zakaah, basi inawajibika katika mali yake kwanza kutolewa deni la Zakaah, tena iwe kabla ya kutimizwa wasia alioacha na kabla ya urithi kugawiwa.
Allaah Anasema:
مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِي بِهَا أَوْ دَيْنٍ ۗ
"Baada ya kutoa wasia aliousia (maiti) au kulipa deni". [An-Nisaa: 11]
Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Deni la Allaah linastahiki zaidi kulipwa". Na Zakaah ni deni la Allaah.
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:
“Mtu mmoja alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
"Mama yangu amefariki na anadaiwa saumu ya mwezi mzima, je nimlipie?"
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza:
"Mama yako angelikuwa na deni ungemlipia?"
Akasema:
"Ndiyo, ningemlipia".
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
"Basi deni la Allaah linastahiki zaidi kulipwa". [Al-Bukhaariy na Muslim]
NA ALLAAH ANAJUA ZAIDI
Maoni
Chapisha Maoni