Uchawi na Hukmu zake

 UCHAWI   NA   HUKMU ZAKE


Nini Maana Ya Uchawi?

 

Al Azhari ambaye ni mtungaji wa kamusi maarafu ya kiarabu iitwayo “LisanulArab” amesema:

 

“Neno “Uchawi”, kwa kiarabu “As Sihr”, maana yake ni kitendo cha kujikurubisha na Shaytwaan na kwa msaada wake (Shaytwaan)”, na akasema pia kuwa; “Uchawi ni kulibadilisha jambo mbali na uhakika wake, nako ni kuwadhihirishia watu jambo lisilo la kweli wakaliona kuwa ni la kweli.” Ama Swahaba Ibni 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

"Uchawi ni kuidhirisha batili katika sura ya haki." Hayo ni katika kamusi za lugha.

 

Amma katika kamusi ya dini, maana ya neno Uchawi (As Sihr), kama alivyofasiri Mwanachuoni mkubwa Fakhruddin Al Razi kuwa:

 

"Ni kila jambo lililofichika sababu zake, linalotokeza kwa sababu zisizo za kawaida na ndani yake mna hadaa (khidaa)."

 

Amma Shaykh Wahiyd Abdulsalaam Bali, mwandishi wa kitabu maarufu kiitwacho 'Al Saarim Al Batar fiy muhaarabat Al Saharatul ashraar', na kitabu kiitwacho "Al wiqaya mina l jinni wa shaytan", ambaye pia ni mtaalamu maarufu katika elimu ya majini na Mashaytwaan na uchawi na ambaye pia ni katika maulamaa maarufu wanaotoa majini kwa njia ya kusoma Qur-aan, yeye anasema:

 

"Uchawi ni makubaliano baina ya mchawi na Jinni akishurutishwa mchawi kufanya mambo ya haramu au ya shirki, na baada ya kufanya hayo, Jinni anashurutishwa kumsaidia na kumtii mchawi huyo kwa kila anachotaka."

 

Baadhi ya yale ambayo mchawi anatakiwa na Shaytwaan ayatende ili ajikurubishe naye ni:

 

· Mchawi anatakiwa auvae msahafu miguuni na aingie nao chooni

· Aandike baadhi ya aayah za Qur-aan kwa damu ya hedhi.

· Miongoni mwao wanashurutishwa kuandika aya za Qur-aan penye nyayo za miguu.

· Au aiandike suwrah Al-Faatihah kinyume nyume.

· Asali bila ya Udhuu.

· Wengine hutakiwa kuchinja mnyama bila ya kulitaja jina la Allaah kisha amtupe mnyama huyo mahali maalum anapoamrishwa na Shaytwaan.

· Wamo miongoni mwao wanaozungumza na nyota au kuzisujudia.

· Au hutakiwa kuandika herizi kwa maneno yenye kufru ndani yake

 

Imeelezwa kwamba katika nchi ya Sham kulikuwa na mtu ambaye watu walikuwa wakimpenda na kumheshimu sana wakimdhania kuwa ni mtu mwenye makarama.

 

Mtu huyu alikuwa kila mwaka katika msimu wa Hajj akiwatumikia watu wa mji wake kwa kuchukua barua zao na vitu vyao na kuwapelekea watu wao waliokwenda Saudia kuhijji. Alikuwa akipeleka na kurudi kwa muda wa siku moja au mbili tu, na watu walimpenda sana na kuamini kwamba alikuwa ni Waliy.

 

Siku moja mtu huyo aliumwa sana, akamuita mwanawe na kumwambia kuwa kama atakufa, basi ende mahali fulani wakati wa usiku na atamkuta ngamia wa aina fulani na ampande na kufuata amri zote atakazopewa na ngamia huyo.

 

Alipofariki dunia, mwanawe alifanya kama alivyoambiwa na baba yake, akaondoka peke yake wakati wa usiku na kuelekea jangwani kule alikoambiwa na baba yake kuwa atamkuta ngamia. Akamkuta ngamia kama alivyoambiwa, akampanda na alipokuwa akenda, ngamia akaanza kusema na kumtaka kijana yule ashuke na amsujudie.

 

Yule kijana alishtuka sana kusikia ngamia akisema na pia akashangazwa na amri zake, akamwambia:

"Vipi nikusujudie, kweni wewe ni nani?"

"Ikiwa unataka nifuate amri zako kama nilivyokuwa kwa baba yako, na nikupeleke popote utakapo duniani, basi unisujudie kama alivyokuwa akinisujudia baba yako."

Yule kijana akajibu:

"Mimi ninamsujudia Allaah peke yake, amma wewe la, siwezi kukusujudia."

Ngamia akamrusha kijana yule kutoka juu ya mgongo wake na kumwangusha chini, na kijana yule akatoka mbio mpaka nyumbani kwa mama yake na kumuelezea yote aliyoyaona na kwamba baba yake alikuwa akimsujudia Jinni ndiyo maana alikuwa na uwezo wa kusafiri kila anapotaka kwenda kwa kupaishwa na jini yule.

 

Kwa haya inatubainikia kuwa Jinni hamsaidii wala hamhudumii mchawi wala mtu yeyote isipokuwa naye kwa mkabala wake atumikiwe kwa kutendewa matendo ya kufru, na ‘ulamaa wanasema:

 

"Kila mchawi anapokufuru zaidi, basi Shaytwaan humtumikia kwa nguvu zaidi, na mchawi akitaka apate huduma ya hali ya juu kabisa kutoka kwa masultani wa majini au kwa kiarabu wanaitwa "Maradatul Jinni", basi inambidi afanye kufuru kubwa zaidi, na kwa ajili hiyo, mchawi anapotaka nguvu juu ya wenzake inamlazimikia akufuru zaidi."

Kutokana na haya tunafahamu kwamba mchawi na Shaytwaan ni marafiki na washirika katika kumuasi Allaah.

 

Allaah Anasema:

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ قَدِ اسْتَكْثَرْتُم مِّنَ الْإِنسِ ۖ وَقَالَ أَوْلِيَاؤُهُم مِّنَ الْإِنسِ رَبَّنَا اسْتَمْتَعَ بَعْضُنَا بِبَعْضٍ وَبَلَغْنَا أَجَلَنَا الَّذِي أَجَّلْتَ لَنَا ۚ قَالَ النَّارُ مَثْوَاكُمْ خَالِدِينَ فِيهَا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۗ إِنَّ رَبَّكَ حَكِيمٌ عَلِيمٌ ﴿١٢٨﴾

Na Siku Atakapowakusanya wote (Allaah Atasema):  Enyi hadhara ya majini! Kwa yakini mmetafuta kwa wingi (kuwapotoa) katika wana Aadam. Na watasema marafiki wao wandani katika wana Aadam: Rabb wetu! Tulinufaishana baadhi yetu na wengineo, na tumefikia muda wetu ambao Umetupangia. (Allaah) Atasema: Moto ndio makazi yenu, ni wenye kudumu humo, isipokuwa Atakavyo Allaah. Hakika Rabb wako ni Mwenye hikmah wa yote, Mjuzi wa yote. [Al-An'aam: 128]

  

Vipi Utaweza Kumjua Mchawi?

 

Zifuatazo ni dalili zitazokuwezesha kutofautisha baina ya mganga na mchawi. Utakapoona mojawapo ya dalili zufuatazo utambuwe kuwa huyo ni mchawi bila shaka yeyote na wala si shekhe au mganga:-

 

· Mchawi huuliza jina la mgonjwa na jina la mama yake

· Huchukua baadhi ya vitu vya mgonjwa kama vile nguo za nje au za ndani au kitambaa cha kufutia jasho n.k.

· Hutaka mnyama mwenye sifa maalum au rangi maalum ili achinjwe na hapigiwi BismiLLaahi anapochinjwa

· Huandika hirizi

· Husema maneno yasiyojulikana

· Humtaka mgonjwa aepukane na watu muda maalum na akae katika chumba kisichofikiwa na juwa

· Mara nyengine humtaka mgonjwa asiguse maji muda wa siku arubaini hivi (anasema Shaykh Wahiyd Abdulsalaam Bali kwamba akikutaka ufanye hivyo ujue kwamba Jinni anayemtumikia mchawi huyo ni mkiristo)

· Humpa mgonjwa vitu ili avifukie ardhini

· Humpa mgonjwa karatasi aziunguze kisha ajifukize na moshi wake

· Mara nyengine humwambia mgonjwa jina lake na mji anaoishi

· Huandika maneno katika karatasi na kumwambia mgonjwa azichemshe na kunywa maji yake

UKIONA DALILI HIZI KWA MGANGA UMJUE HAPO HAPO KUWA NI MCHAWI NA UEPUKANE NAYE

 

Anasema Shaykh Wahiyd Abdulasalaam Bali:

 

"Ukiutizama uso wa mchawi utakiona kiza cha kufru kilivyotanda katika uso huo mfano wa mawingu meusi.”

 

Anaendelea kusema Shaykh huyo:

“Kwa wale wanaowajua wachawi, wanawaona siku zote wakiwa katika dhiki, shida, matatizo katika siha zao, matatizo na wake zao au watoto wao na siku zote hawana raha wala utulivu.”

Allaah Anasema:

وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِّنَ الْإِنسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِّنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا

Na kwamba walikuwa wanaume miongoni mwa wana Aadam wanajikinga na wanaume miongoni mwa majini, basi wakawazidishia madhambi, uvukaji mipaka ya kuasi na khofu. [Al-Jinn: 6]

 

Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا

Na atakayejitenga na ukumbusho Wangu basi hakika atapata maisha ya dhiki.., [Twaahaa: 124]

  

Dalili Kuwa Uchawi Upo, Kutoka Katika Qur-aan Na Katika Sunnah (mafundisho Ya Nabiy (swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Sallam)

 

Katika Suwrah Yunus aayah ya 77 Allaah Anasema:

قَالَ مُوسَىٰ أَتَقُولُونَ لِلْحَقِّ لَمَّا جَاءَكُمْ ۖ أَسِحْرٌ هَـٰذَا وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُونَ﴿٧٧﴾

Muwsaa akasema: Je, mnasema kuhusu haki ilipokujeni? Hii ni sihiri? Na wachawi hawafaulu. 

 

Hii ni dalili kwamba uchawi upo na Allaah anatufundisha katika aayah hii kwamba uchawi haufaulu.

 

Na katika suwrah Al-Falaq Akasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ ﴿٤﴾

Na kutokana na shari ya wanaopuliza mafundoni. 

 

Katika kuifasiri aya hii, mmoja katika 'ulamaa wakubwa wa tafsiri ya Qur-aan Imam Al Qurtuby amesema:

 

"Maana ya neno "Naffaathaat", ni wachawi wanapopuliza katika nyuzi huku wakizipiga fundo.”

Na Ibni Kathiyr katika tafsiri yake akinukuu kutoka kwa Ikrimah na Mujahid na Al Hassan Al Basry (Radhwiya Allaahu ‘anhum) amesema:

 

"Hawa wanaopuliza mafundoni ni wachawi, na Allaah anatuamrisha tujiepushe na shari zao.”

 

Amma hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi sallam) zinazotufahamisha kwamba uchawi upo na kwamba uchawi ni katika madhambi makubwa sana, ni hizi zifuatazo:

 

 Kutoka kwa Abi Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

"Jieupusheni na (mambo) saba Yaangamizayo.'

 Wakasema:

'Ni yepi hayo ewe Rasuli wa Allaah?"

Akasema:

"Kumshirikisha Allaah, Uchawi, kuiuwa nafsi iliyoharimishwa na Allaah ila kwa haki yake, kula riba, kula mali ya yatima, kurudi nyuma (kukimbia) katika vita vya Jihadi (huku ukiwaacha wenzio wanapigana), na kuwasingizia uwongo wanawake wema wasio na makosa." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Ndugu yangu Muislamu, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema kuwa mambo hayo 'Yanayomuangamiza', maana yake ni kuwa yanamuangamiza mtu katika moto wa Jahannam

Ukirudia kuisoma tena hadiyth hiyo utaona kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ameutanguliza uchawi kabla ya dhambi ya kuuwa, ingawaje kuuwa ni dhambi kubwa sana, na Allaah Anasema katika Suwrah Al-Nisaa aayah ya 93:

وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا ﴿٩٣﴾

Na atakayemuua Muumini kwa kusudi, basi jazaa yake ni Jahannam, ni mwenye kudumu humo na Allaah Atamghadhibikia na Atamlaani na Atamuandalia adhabu kuu. [Al-Nisaa: 93]

 

Juu ya ukubwa wa dhambi hiyo ya kuuwa, lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) ameipa uzito zaidi dhambi ya Uchawi kwa kuiweka nafasi ya pili baada ya Shirki na kabla ya dhambi ya kuuwa.

 

Soma Bahati Yako (Nyota Yako) Lucky Stars

 

Katika hadiyth ifuatayo iliyosimuliwa na Abu Dawood na Ibni Majah hadiyth ambayo Shaykh Al-Albaaniy ameitaja kuwa ni "hadithi njema", na hadithi hii pia ni dalili kwamba elimu ya kutabiri kwa nyota ambayo huandikwa katika magazeti na watu hupenda kusoma kwa kutaka kujua bahati zao, kitendo hiki ni haramu na yeyote atakayesoma nyota yake, basi swala zake hazikubaliwi kwa muda wa siku arobaini, hii ikiwa anasoma na huku haziamini, amma akisoma na huku anaziamini, basi anaingia katika hukumu ya aliyemuendea mtabiri na kumuuliza jambo, na anakuwa amekwisha kufuru yote aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

"Atakayejifunza sehemu ya elimu ya nyota (utabiri) amejifunza sehemu ya uchawi, akiongeza atakachoongeza (katika uchawi au nyota)."

 

Na hii ni kwa sababu wanaosoma elimu ya nyota (utabiri) wanaamini kwamba katika nyota wanaishi majini ambao ni masultani na wakuu, na wanaitakidi kuwa mambo yetu yote husababishwa na harakati za nyota hizo kila zinapotaharaki kutoka mahali kuelekea pengine. Kwa ajili hiyo wao huzingoja nyota hizo masaa mengi ya usiku ili wapate kuandika talasimu zao, na huku ni sawa na kuziabudu nyota hizo. (Pana tofauti baina ya elimu ya anga za juu (Astronomy) ambayo haina ubaya wowote ndani yake, na elimu ya nyota (Astrology) - utabiri - ambayo ni haramu).

 

Ushahidi Mwengine unapatikana katika hadiyth iliyosimuliwa na Umran bin Hussain (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyesema kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

“Hayuko pamoja nasi mwenye kuamini juu ya nukhsi (waarabu walikuwa wanapotaka kusafiri humrusha ndege na akielekea upande wa kulia basi husafiri, amma akielekea upande wa kushoto huamini ni ukorofi na kuivunja safari yake), na pia hayuko pamoja nasi mwenye kupiga ramli au mwenye kupigiwa, na atakayemuendea mtabiri na akamsadiki asemayo basi kesha kufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)." [Al-Bazaar].

 

Katika hadiyth hizi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) anatukataza tusiwaendee wachawi wala watabiri wa aina yoyote ile kwa kuwauliza juu ya jambo lolote lile, hata kama atajibadilisha na kujiita AlHajj Fulani au Shaykh Fulani au Maalim Fulani au Mganga Fulani na hii ni kutokana na kufru zao wanazozifanya kwa kuwasujudia majini na kuridhishana nao ili wawatumikie.

 

Na hii ni dalili kwamba uchawi upo, maana kama haupo, basi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) asingetukataza kufanya kisichokuwepo.

 

Pia hadiyth hizi zinatufahamisha kwamba mambo haya ni haramu na atakayeyatenda anakuwa amekwishayakanusha yale aliyokuja nayo Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa sababu aliyokuja nayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni kwamba hapana aijuwae ghaibu isipokuwa Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa.

 

Hadiyth ziko nyingi sana, lakini hizi pamoja na aya zilizotangulia zinatosha kuwa ni dalili kwamba yote hayo yametajwa katika Qur-aan na katika mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Uchawi Umeanza Zama Za Nabiy Sulaymaan?

 

Wachawi wanaposoma talasimu zao huwadanganya watu kwa kuanza kusoma baadhi ya aya au sura ndogo ndogo za Qur-aan na kulitajataja jina la Nabii SULAYMAAN na utawasikia daima wanamnasibisha Nabiy huyu ('Alayhis-salaam) na kufru zao hizo ili wajinga wanaowafuata wadhani kwamba hayo yamo katika dini.

 

Uchawi haujaanza zama za Nabiy Sulaymaan kama wachawi wanavyozuwa na kumsingizia Nabii Huyu wa Allaah, bali ulikuwepo kabla yake kwa miaka elfu nyingi.

 

Uchawi ulikuwepo tokea zama za Nabiy Saleh ('Alayhis-salaam) aliyekuja kabla ya Nabii Sulaymaan kwa miaka elfu nyingi.

 

Allaah Anasema:

قَالُوا إِنَّمَا أَنتَ مِنَ الْمُسَحَّرِينَ ﴿١٥٣﴾

Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa. [Ash-Shu'araa: 153]

 

Uchawi Ni Kufru

 

Wachawi na wafuasi wao hupenda kumsingizia Nabiy SULAYMAANI kwa kuinasibisha na kufru yao hiyo na Nabiy huyu mtukufu ambaye Allaah alimpa ufalme ambao hajaupata mwengine baada yake kwa kumpa uwezo wa kuwatiisha majini, upepo, na uwezo wa kujua lugha za wanyama n.k.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

فَسَخَّرْنَا لَهُ الرِّيحَ تَجْرِي بِأَمْرِهِ رُخَاءً حَيْثُ أَصَابَ ﴿٣٦﴾ وَالشَّيَاطِينَ كُلَّ بَنَّاءٍ وَغَوَّاصٍ ﴿٣٧﴾ وَآخَرِينَ مُقَرَّنِينَ فِي الْأَصْفَادِ ﴿٣٨﴾

Basi Tukamtiishia upepo unaokwenda kwa amri yake polepole popote anapotaka kufika. Na mashaytwaan, kila ajengaye na mpiga mbizi. Na wengineo, wafungwao minyororoni. [Swaad: 36-38]

 

Katika tasfiri yake, Ibni Kathiyr amenukuu kauli ya Ibni 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

 

"Asif - alikuwa mwandishi wa Nabiy Sulaymaan na alikuwa akilijuwa jina tukufu la Allaah (Al ismul aadham), na alikuwa akiandika kila kitu katika daftari kwa amri ya Nabiy Sulaymaan na kulificha daftari hilo chini ya kiti cha Nabiy Sulaymaani. Alipofariki Nabiy SULAYMAAN, majini wakayatoa maandishi hayo wakachanganya na kuandika baina ya kila mistari miwili uchawi na kufru yao, kisha wakawaambia watu wao kuwa hayo ndiyo maandishi ya Nabiy Sulaymaan na ndiyo aliyokuwa akiyatenda, na Mayahudi wakayasadiki maneno hayo, wakawa wanamtangazia Nabii huyu kuwa ni mchawi.

 

Mpaka alipokuja Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kuteremshiwa aya ya 102 katika Suwrah Al-Baqarah:

 

Allaah Anasema:

 

وَاتَّبَعُوا مَا تَتْلُو الشَّيَاطِينُ عَلَىٰ مُلْكِ سُلَيْمَانَ ۖ وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ وَلَـٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ وَمَا أُنزِلَ عَلَى الْمَلَكَيْنِ بِبَابِلَ هَارُوتَ وَمَارُوتَ ۚ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ ۖ فَيَتَعَلَّمُونَ مِنْهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِ بَيْنَ الْمَرْءِ وَزَوْجِهِ ۚ وَمَا هُم بِضَارِّينَ بِهِ مِنْ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ ۚ وَلَقَدْ عَلِمُوا لَمَنِ اشْتَرَاهُ مَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ ۚ وَلَبِئْسَ مَا شَرَوْا بِهِ أَنفُسَهُمْ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿١٠٢﴾ 

Na wakafuata yale waliyoyasoma mashaytwaan juu ya ufalme wa Sulaymaan; na Sulaymaan hakukufuru lakini mashaytwaan ndio waliokufuru; wanafundisha watu sihiri na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili katika (mji wa) Baabil; Haaruwt na Maaruwt. Nao wawili hawamfundishi yeyote mpaka waseme: Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru. Kisha wakajifunza kutoka kwa hao wawili yenye kupelekea kufarikisha kwayo baina ya mtu na mkewe. Na wao hawawezi kamwe kumdhuru yeyote kwayo isipokuwa kwa idhini ya Allaah; na wanajifunza yanayowadhuru na wala hayawanufaishi; na kwa yakini walijua kwamba atakayechuma haya hatopata katika Aakhirah fungu lolote, na ni ubaya ulioje walichojiuzia nafsi zao, lau wangelikuwa wanajua. [Al-Baqarah: 102]

  

Katika aayah hii Allaah anatufahamisha pia kuwa uchawi ulikuwepo kabla ya Nabiy Sulaymaan kwa miaka mingi, tokea zama za ustaarabu wa Babiloni walipoteremshwa Malaika wawili, Haruta na Maruta ili kuwaonyesha watu na kuwafahamisha nini uchawi, wapate kuujuwa mara watakapouona na wasiufuate, na hii ni kwa sababu uchawi ni kufru.

 

Watu waliacha kufuata nasaha za Malaika hao na wakajifunza yale ambayo yatawadhuru na wala hayatawafaa, ingawaje walikuwa wakijuwa kuwa aliyekhiari haya hatakuwa na sehemu yoyote katika Akhera.

 

Wachawi mpaka hivi sasa wanajaribu kuunasibisha uchawi wao na Nabiy Sulaymaan pamoja na Malaika hawa wawili.

 

Tatizo kubwa hupatikana pale wachawi wanapofanya uganga wao pale wanaposema maneno yao ya kichawi. Wao huchanganya maneno hayo na baadhi ya aayah za Qur-aan na wanaofanyiwa uganga hudhania kwamba Qur-aan ndiyo inayosomwa na kwa ajili hiyo na kutokana na ujinga wao, huhadaika na kujiingiza nao katika shirki.

  

Hukumu Ya Uchawi Katika Dini Ya Kiislamu

 

Anasema Imam Maalik (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake AlMuwata:

 

"Mchawi anayefanya uchawi mwenyewe, hukumu yake ni kuuwawa, ama yule anayemuendea mchawi, huyo hauwawi."

 

Ibni Qudama naye anasema:

 

"Hukumu ya mchawi ni kuuawa."

 

Hukmu kama hizi pia zimepokelewa kutoka Swahaba mbali mbali kama vile Umar, Uthmaan, Ibni 'Umar na wengine (Radhwiya Allaahu anhum).

 

Hukumu hii ya kuuwawa kwa mchawi pia ameitamka Imam Ahmed bin Hambal (Rahimahu Allaah).

 

Na imepokelewa kutoka kwa Swahaba mbali mbali kwamba Umar bin Al-Khataab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliwaandikia Swahaba kuwaamrisha wamuuwe kila mchawi mwanamke au mwanamume. Anasema mmoja katika Swahaba kwamba baada ya kupata maandishi hayo waliwakamata na kuwaua wachawi watatu."

 

Amma Imam Shafi (Rahimahu Allaah), yeye anaona kuwa mchawi asiuliwe isipokuwa akikiri mwenyewe kwamba ameuwa kwa uchawi wake.

 

Kutokana na yaliyotangulia infahamika kwamba Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhu) pamoja na ‘ulamaa wengi wanaona kwamba hukumu ya mchawi ni kuuliwa, isipokuwa Imam Ash-Shaafi'y (Rahimahu Allaah), yeye anaona kuwa auliwe tu ikiwa mchawi huyo atakiri kwamba ameuwa kwa uchawi wake.

 

Kujikinga Na Shari Za Wachawi Na Majini Wao

 

Zifuatazo ni baadhi ya Njia za kujikinga na waovu hao:

  

Kusafisha Nia

 

Ibilisi alipohukumiwa kupotea kwa sababu ya kuasi kwake, aliahidi kuwapoteza viumbe wote isipokuwa wale waliosafika kikweli.

 

Ibilisi akasema kumwambia Allaah:

إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ﴿٤٠﴾

Isipokuwa waja Wako miongoni mwao waliokhitariwa kwa ikhlaasw zao. [Al-Hijr: 49]

 

Kusafisha nia (Al-Ikhlas), maana yake ni kuzihusisha Ibada zote kwa moyo wote kwa ajili ya Allaah peke yake, siyo kujionyesha mbele za watu kuwa ni Mcha wa Allaah na unapokuwa peke yako unamuasi.

 

Al Junaid, mmoja katika maulamaa wakubwa wa wakati wake amesema:

 

"Allaah ana waja wake wenye akili, walipopata akili wakaifanyia kazi, walipofanya kazi wakaitakasa kazi hiyo na kule kuitakasa kwao kukawaingiza katika milango ya kheri yote."

 

Kutia Udhu

 

Katika hadiyth nyingi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ametufundisha juu ya umuhimu wa kubaki na udhu kila mtu anapoweza kwa ajili ya kupata thawabu na kwa ajili ya kujikinga na kila shari.

 

Swala Katika Jamaa

 

Kuswali swala za jamaa msikitini, maana Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kwamba mbwa mwitu (Shaytwaan) huwala kondoo wanaotembea mbali na wenzao.

 

Swala Za Sunnah

 

Swala za Sunnah uziswali nyumbani, usiiache nyumba yako ikawa kama kaburi, na unaposwali nyumbani Shaytwaan hulia na kutoka nje ya nyumba yako huku akisema;

"Sina pa kulala humu, wala sina pa kula humu".

  

Kumuomba Allaah

 

Kumuomba Allaah kila mara Shaytwaan anapotaka kukuchezea na kila unapoingia mahali pachafu. Kwa mfano:

 

Unapoingia chooni uisome dua ifuatayo:

 

"Allaahumma inniy audhu bika minal khubuthi wal khabaaith). Na maana yake; (Allaah mimi najikinga kwako kutokana na majini wanaume na majini wanawake).

 

Kabla ya kulala usome Suwrah Al-Ikhlaas, Suwrah Al-Falaq na Suwrah Al-Naas pamoja na Ayatul Kursy, maana hadiyth sahihi tuliyoitaja mwanzo wa darsi hii inasema kuwa anayeisoma aayah hii, Allaah anaendelea kumhifadhi mpaka asubuhi anapoamka.

 

Ni vizuri pia kuzisoma aya tano za mwanzo za Suwrah Al-Baqarah kisha Ayatul Kursy kisha kuzisoma aya tatu za mwisho za Suwrah Al-Baqarah na Allaah Atakulinda na majini pamoja na uchawi katika siku nzima.

 

Kuzisoma dua mbali mbali kama vile:

(Audhu bikalimati Allaahi ttaamah min kulli shaytanin wa haammah wa min kulli aynin laammah).

Na maana yake ni;

"Najikinga kwa Allaah kutokana na kila Shaytwaan na (kila) mdudu anayesota (kama vile nge na nyoka nk. na kwa kila jicho linalodhuru).

(BismiAllaahi lladhiy laa yadhuru ma-a smihiy shayun fil ardhi walaa fiy ssamaa wahuwa ssamiyl aliym).

Unapotoka nje ya nyumba usome:

(BismiAllaah tawakkaltu ala Allaah walaa haula walaa quwwata illa biAllaah)

                               

Kusoma Qur-aan

 

Qur-aan ni kinga kubwa sana, na Muislamu anatakiwa daima awe anaisoma nyumbani kwake.

Hapana kitukufu anachokiogopa Shaytwaan kuliko Qur-aan, dua, pamoja na Ibada zinazokusogeza karibu na Rabb wako. Na kila mtu anapokuwa mbali na Rabb wake anakuwa karibu sana na Shaytwaan.

 

kupiga mfano:

 

Mtu anapita njiani akakumbana na mbwa mkali anayebweka huku akiwa amemzuwilia njia. Bila shaka mtu huyo atashindwa na hila ya kumuondosha ili apite na zake; bali ataogopa asitafunwe na mbwa huyo. Lakini mtu huyo mara atakapotambua kuwa mwenye mbwa huyo yupo karibu, na kwamba akimuomba amwondoe njiani basi kwa ukelele wake mmoja tu, mbwa huyo ataondoka taratibu na kumpisha apite, bila shaka atamuomba msaada wake.

Mfano huu ni mfano wako wewe binadamu unapomuomba Rabb wako akukinge na Mashaytwaan.

 

Dua Zinamkumba Shaytwaan

 

Kama vile Shaytwaan anavyoweza kuwakumba wanadamu walioghafilika na kumdhukuru Allaah, Shaytwaan naye pia hukumbwa na dua za wanaomdhukuru Allaah:

 

Imeelezwa na ‘ulamaa kuwa, Shaytwaan anapojaribu kumsogelea mcha wa Allaah mwenye kumdhukuru Rabb wake kila wakati kwa ajili ya kumkumba, basi dua zake humkumba Shaytwaan huyo na kumuangusha chini. Kisha Mashaytwaan wenzake hukusanyika na kuulizana:

"Amepatwa na nini huyu?"

Wenzao huwajibu:

"Amekumbwa na binadamu."

 

Dhikru Allaah

 

Kwa kumaliza napenda kujikumbusha nafsi yangu kwanza na pia kuwakumbusha ndugu zangu Waislamu pia kwamba, hakuna kinga kubwa inayomkinga mtu kutokana na kila balaa baada ya Qur-aan kama kumdhukuru Allaah.

 

Kumdhukuru unapolala, unapoamka, unapotoka nyumbani, unapositushwa na jambo, unapofurashishwa. Katika kila jambo lako jema au lisilo jema, bali hata katika kumuasi Rabb wako unapomkumbuka Allaah na kukumbuka uwezo Wake juu yako na neema Zake juu yako mara utayaacha maasi hayo.

 

Na ukumbuke kwamba kwa msaada wake Yeye tu Subhanahu wa Ta’aalaa utaweza kujikinga na kila balaa.

 

Usiingize Ndani Ya Nyumba Yako Yafuatayo:

 

Mwisho kabisa ningependa kukumbusha kuwa ndani ya nyuma yako usije ukaingiza yafuatayo;

Usitundike picha yeyote ile.

Usisikilize nyimbo.

Usiweke baraza za kusema watu au kutukana watu.

Usitizame filam za sinema nk.

Hayo yote yanakaribisha Mashaytwaan katika nyumba yako na yanafukuza Malaika.

 

Allaah Anasema:

وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ ۚ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٢٠٠﴾ إِنَّ الَّذِينَ اتَّقَوْا إِذَا مَسَّهُمْ طَائِفٌ مِّنَ الشَّيْطَانِ تَذَكَّرُوا فَإِذَا هُم مُّبْصِرُونَ ﴿٢٠١﴾

Na pindi utakapokuchochea uchochezi kutokana na shaytwaan; basi omba kinga kwa Allaah. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. Hakika wale waliokuwa na taqwa inapowagusa pepesi za shaytwaan hukumbuka, basi mara wao huwa wenye kuona kwa utambuzi. [Al-A'araaf: 200-202]

 

Hivi ndivyo ilivyo, wale wanaoasi daima hawapendi kuona wenziwao wanaokoka na wanajaribu kila njia kuwavutia katika maasi, lakini Mwenye kuomba msaada wa Allaah basi Rabb wake Atamuokoa.


NA  ALLAAH  ANAJUA ZAIDI

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Eda: Maana ya Eda, Hikma ya Eda , Hukmu zake, Mambo yanayopasa na uyasiyopasa kwa mwenye Eda

Namna ya Kuswali Swalat Kusuwf (Swalah ya Kupatwa kwa Jua/Mwezi

Ramadhwaan ni Mwezi wa Du’aa na Du’aa hutakabaliwa