Maana ya Zakaah
MAANA YA ZAKAAH
Assallaam Aleykum Warahmatullaah Wabarakatuh
Kutoa Zakaah ni nguzo ya tatu ya Islam.Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Nguzo za Uislaam ni tano. Shahada kuwa hapana muabudiwa wa haki ila Allaah, na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, na Kusimaamisha Swalaah, na Kutoa Zakaah, na Kufunga mwezi wa Ramadhwaan na Kuhiji Makkah kwa mwenye uwezo wa kufika huko".
Kufaridhishwa kwa Zakaah ni jambo muhimu na tukufu sana kwa Waislam kwa sababu ya wingi wa faida yake na kwa ajili ya haja kubwa ya kuwepo kwa jambo hilo, kutokana na masikini na mafakiri wanaohitajia sana msaada wa ndugu zao wenye uwezo, kwani katika Kutoa Zakaah uhusiano mzuri unajengeka baina ya Waislam matajiri na Waislam masikini, na hii ni kwa sababu siku zote moyo wa mtu huelekea na kumpenda yule anayemfanyia wema na ihsani. Zakaah inasaidia pia katika kuzisafisha na kuzitakasa nyoyo.
Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا
Chukua (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo. [At-Tawbah: 103]
Katika kutoa Zakaah au Swadaqah kunaizoesha nafsi katika kuwapendelea kheri watu wenye haja na katika kuwaonea huruma na pia kunaipatia nafsi baraka nyingi kutoka kwa Allaahu Subhanaahu wa Ta’aalaa.
Allaah Anasema:
وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ
Na kitu chochote mtoacho, basi Yeye Atakilipa, Naye ni Mbora wa wenye kuruzuku. [Sabaa: 39]
Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Allaahu Anasema: 'Ee mwana Aadam, toa na sisi tutakupa"
Anasema Ibn Uthaymiyn:
"Kutoa Zakaah ni jambo liliofaradhishwa katika Uislam, na ni nguzo muhimu sana baada ya Shahada mbili na Swalaah, na dalili ya kuwajibika kwake imo ndani ya Qur-aan na pia katika mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), pamoja na ijmai ya Waislam, na yeyote anayeikanusha nguzo hii anakuwa Kafir aliyertadi katika Uislaam, na hukumu yake ni kutubishwa, na akitubu anasamehewa. Ama akikataa kutubu na akaendelea kuikanusha basi hukmu yake ni kuuliwa. Ama anayeifanyia ubakhili au akapunguza katika Zakaah yake, huyo anakuwa miongoni mwa madhalimu wanaostahiki adhabu ya Allaahu.
Allaahu Anasema:
وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ
Na wale wanaorundika dhahabu na fedha na wala hawazitoi katika njia ya Allaah, basi wabashirie adhabu iumizayo. Siku zitakapopashwa katika Jahannam, na kwazo vikachomwa moto vipaji vyao, na mbavu zao, na migongo yao (wakiambiwa): Haya ndiyo mliyoyarundika kwa ajili ya nafsi zenu. Basi onjeni yale mliyokuwa mkiyarundika. [At-Tawbah - 34 - 35]
"Miongoni mwa faida za kutoa Zakaah anazozipata mtu katika dini yake" anaendelea kusema Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah), "Ni kuitimiza nguzo katika nguzo za Kiislam, jambo litakalomletea mtu furaha katika dunia yake na katika akhera yake, na pia inazidi kumkaribisha mja kwa Rabb wake na kumuongezea Imani, kama ilivyo katika mambo yote ya kumtii Allaahu Subhanaahu wa Ta’aalaa."
Maana ya Zakaah
Zakaah ni ile haki Aliyoifaradhisha Allaah kwa Muislam katika mali yake anayotakiwa kuwapa wanaostahiki.
Neno Zakaah, katika lugha (katika kamusi ya lugha ya Kiarabu) maana yake ni 'Kujitakasa', kwa sababu anayetoa Zakaah anataraji kuitakasa mali yake, nafsi yake na kupata baraka kutoka kwa Rabb wake.
Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا
Chukua (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo. [At-Tawbah: 103]
Zakaah ni nguzo ya tatu ya Uislaam iliyofaradhishwa katika Qur-aan tukufu na katika mafundisho ya Nabiy mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwa sababu ya umuhimu wake, Allaah ameitaja mara themanini na mbili katika Qur-aan kwa kuifuatanisha pamoja na Swalaah.
Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:
"Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomteua Muadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa gavana wa nchi ya Yemen na kadhi wao alimwambia:
"Unakwenda katika nchi ya watu wa Ahlul Kitab, kwa hivyo (kwanza) walinganie katika shahada ya Laa ilaaha illa Allaah na kwamba mimi ni Rasuli wa Allaah, wakitii juu ya hilo, wafundishe kuwa Allaah amewafaradhishia Swalaah tano mchana na usiku, wakitii juu ya hilo, wafundishe kuwa Allaah amewafaradhishia Swadaqah (Zakaah) za mali zao, zichukuliwe kutoka kwa matajiri wao na kurejeshewa masikini wao, na kama wakitii juu ya hilo, usije ukachukuwa mali zao zenye thamani, na uiogope dua ya aliyedhulumiwa, kwani hapana kizuizi baina yake (dua hiyo) na baina ya Allaah". [Imesimuliwa na Ma-Imaamu wote wa Hadiyth]
Imesimuliwa pia na At-Twabaraaniy kutoka kwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Allaah amewafaradhishia matajiri wa Kiislam katika mali zao kiasi cha kuwatosha masikini wao. Na (masikini) wasingepata tabu ya njaa na mavazi isipokuwa kutokana na ubakhili wa matajiri wao. Jueni kuwa Allaah atawahesabia hesabu nzito sana na atawapa adhabu iumizayo".
Na Allaah anajua zaidi
Maoni
Chapisha Maoni