Maana ya Jini

 MAANA YA JINI na KWANINI AITWE JINI



 

Jina Lake

 

Ameitwa JINNI kwa sababu ya kutokuonekana kwake na watu, na hii ni kwa sababu kila kisichoonekana kwa jicho la binadamu katika lugha ya kiarabu jina lake hutokana (hutoholewa) na herufi mbili hizi; (Jiym) na (Nuun).

 

Kwa mfano; 'Bustani' huitwa 'Jannakwa sababu ya kuzungukwa kwake na majani kila upande pasiweze kuonekana ndani. Elimu ya uzazi huitwa 'Ilmul ajinna', kwa sababu ya kutokuonekana kwa kile kilichokuwemo tumboni mwa mzazi. Hata mwendawazimu naye huitwa 'majinunkwa sababu ya kutoweka kwa akili yake. Na Majinni nao wamepewa jina hilo kwa sababu ya kutokuonekana kwao kwa macho ya binadamu.

 

Ukichunguza utaona kuwa maneno yote hayo; 'Janna, ajinna, majinun, jinni', yana herufi ya 'Jiym na Nuun' ndani yake.

 

Imani Juu Ya Ghaibu

 

Kuamini juu ya ghaibu (yasiyoonekana) ni katika misingi ya itikadi ya Dini.

 

Allaah Anasema:

 الم ﴿١﴾ ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ ۛ فِيهِ ۛ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ ﴿٢﴾ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٣﴾

"Alif Laam Miym. Hiki ni kitabu kisicho na shaka ndani yake, ni mwongoz kwa wenye taqwa. Ambao huamini ya ghayb na husimamisha Swalaah na katika vile Tulivyowaruzuku hutoa. [Al-Baqarah: 1-3]

 

Katika aya hizi, Allaah ametaja baadhi ya sifa za wachaji Allaah ikiwemo ikiwemo sifa hii ya kuamini Ghaibu.

 

Na maana ya neno 'Ghaibu', ni yale tusiyoweza kuyaona tuliyofundishwa na Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa au Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Ushahidi Wa Kuwepo Majini Katika Qur-aan Tukufu

 

Katika Qur-aan Allaah Anasema:

وَإِذْ صَرَفْنَا إِلَيْكَ نَفَرًا مِّنَ الْجِنِّ يَسْتَمِعُونَ الْقُرْآنَ فَلَمَّا حَضَرُوهُ قَالُوا أَنصِتُوا ۖ فَلَمَّا قُضِيَ وَلَّوْا إِلَىٰ قَوْمِهِم مُّنذِرِينَ﴿٢٩﴾

Na pale Tulipowaelekeza kwako (ee Muhammadصلى الله عليه وآله وسلم  ) kundi miongoni mwa majini wakisikiliza kwa makini Qur-aan;  [Al-Ahqaf: 29]

 

Na Akasema:

يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ أَلَمْ يَأْتِكُمْ رُسُلٌ مِّنكُمْ يَقُصُّونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِي

Enyi hadhara ya majini na wana Aadam! Je hawajakufikieni Rusuli miongoni mwenu wanakusimulieni Aayaat Zangu.. [Al- An’aam: 130]

 

Ushahidi Wa Kuwepo Kwa Majina Katika Mafundisho Ya Nabiy (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihi Wa Sallam) ‘Sunnah’

 

Katika 'Sunnah', (mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), wameelezea [Imam Al-Bukhaariy na Muslim] katika vitabu vyao vilivyo sahihi kwamba Ibni 'Abbaas (Radhwiya Allaahu anhu) amesema:

 

"Majinni waliposhindwa kupata siri kutoka mbinguni na wakawa wanafukuzwa kwa vimondo kila wanapojaribu kuzisogelea mbingu, wakarudi makwao. Na jamii zao walipotaka kujua sababu ya kurudi kwao huko na kushindwa kwao kupata siri za mbinguni, maana kabla ya hapo walikuwa wakiweza kupata baadhi ya habari za huko, wakawajibu:

 

"Pamewekewa vizuizi baina yetu na baina ya (kupata) habari za mbinguni".

Wenziwao wakasema:

 

"Bila shaka pana jambo kubwa lililotokea, tembeeni ardhi yote Mashariki na Magharibi mtafute ni kitu gani kilichokuzuwieni msiweze kupata habari za mbinguni.”

 

Walipofika mahali paitwapo; “Soko la Akadha”, waislamu walikuwa wakiswali Swala ya Alfajiri, na majini hao wakaisikia Qur-aan ikisomwa, ndipo waliposema:

 

"Hii (Qur-aan) wAllaahi, ndiyo iliyokuzuwieni msiweze kupata habari za mbinguni."

Wakarudi kwa watu wao na kuwaambia:

 

"Enyi jamii yetu! “Hakika sisi tumesikia Qur-aan ya ajabu"Allaah Amesema katika Suwrah Jinn aayah ya mwanzo:

قُلْ أُوحِيَ إِلَيَّ أَنَّهُ اسْتَمَعَ نَفَرٌ مِّنَ الْجِنِّ فَقَالُوا إِنَّا سَمِعْنَا قُرْآنًا عَجَبًا﴿١﴾

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Nimefunuliwa Wahy kwamba kundi miongoni mwa majini lilisikiliza; wakasema: ‘Hakika sisi tumeisikia Qur-aan ya ajabu. [Al-Jinn: 1]

 

Hizi ni dalili zilizo wazi za kuwepo kwa viumbe hawa, na kukanusha kuwepo kwao kwa sababu ya kutokuonekana kwao si hoja maana vitu vingi hatuvioni na tunakubali kwamba vipo kutokana na athari zake. Kwa mfano, joto, baridi, umeme nk. Hivi vyote hatuvioni lakini tunakubali kuwepo kwake baada ya kuona athari zake.

 

Dalili Katika Qur-aan Kuwa Jinni Ameumbwa Kwa Moto

 

Ndani ya Qur-aan mna dalili nyingi zinazotujulisha kuwa Jinni ameumbwa kwa moto, na tutazitaja baadhi ya dalili hizo:

 

Allaah Amesema:

قَالَ مَا مَنَعَكَ أَلَّا تَسْجُدَ إِذْ أَمَرْتُكَ ۖ قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ ﴿١٢﴾

(Allaah) Akasema: Nini kilichokuzuia usisujudu Nilipokuamrisha? (Ibliys) Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, na yeye Umemuumba kwa udongo. [Al-A’raaf: 12]

 

Na Akasema:

وَخَلَقَ الْجَانَّ مِن مَّارِجٍ مِّن نَّارٍ ﴿١٥﴾

Na Akaumba majini kutokana na mwako wa moto. [Ar-Rahman: 15]

 

Dalili Katika Mafundisho Ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Kuwa Jinni Ameumbwa Kwa Moto

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ametujulisha pia kuwa Majini wameumbwa kwa moto, na tutataja baadhi ya kauli zake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

"Wameumbwa Malaika kwa nuru na Majini kwa ndimi za moto na Adam ameumbwa kwa mliyokwisha elezewa (Udongo)." [Muslim]

 

Majini Wanazaliana

 

Allaah Anasema:

أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ ۚ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلًا ﴿٥٠﴾

Je, basi mnamfanya yeye na kizazi chake walinzi pasi Nami; na hali wao kwenu ni maadui? Ubaya ulioje mbadala huu kwa madhalimu.   [Al-Kahf: 50]

 

Kauli ya Allaah katika aya hii pale aliposema 'Na Kizazi Chake'. inamaanisha kwamba majini wanazaliana.

 

Wameumbwa Kabla Ya Binadamu

 

Allaah Anasema:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ﴿٢٦﴾وَالْجَانَّ خَلَقْنَاهُ مِن قَبْلُ مِن نَّارِ السَّمُومِ﴿٢٧﴾

Na kwa yakini Tumemuumba insani kutokana na udongo wa mfinyanzi unaotoa sauti, unaotokana na tope nyeusi iliyotaghayari. Na majini Tuliwaumba kabla kutokana na moto ulio mkali mno. [ Al-Hijr: 26-27]

 

Kwa hivyo majini waliumbwa kabla yetu na waliishi katika ardhi hii hata kabla ya kuumbwa kwa Aadam ('Alayhis-salaam), na hii ndiyo maana Allaah alipowaarifu Malaika kuwa anataka kuumba viumbe katika ardhi wakasema:

قَالُوا أَتَجْعَلُ فِيهَا مَن يُفْسِدُ فِيهَا وَيَسْفِكُ الدِّمَاءَ

Utaweka humo atakayefanya ufisadi humo na kumwaga damu.., [Al-Baqarah: 30]

 

Malaika waliuliza suala hili si kwa ajili ya kupinga amri ya Allaah au kwa kumuonea wivu mwanadamu, bali waliuliza kwa ajili ya kutaka kuijua hekima ya kuumbwa viumbe hawa, na hii ni kwa sababu walielewa kutokana na viumbe vilivyotangulia vilivyoishi ardhini, kwamba vina sifa ya ufisadi na umwagaji wa damu.

 

Anasema Ibni Kathiyr (huyu ni katika ‘Ulamaa na mfasiri mkubwa wa Qur-aan) kwamba kabla ya kuumbwa kwa wanadamu, Majinni na viumbe wasiokuwa wanadamu walikuwa wakiishi ardhini na kwamba walikuwa wakifanya ufisadi mkubwa pamoja na umwagaji wa damu.

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

"Majinni waliishi ardhini kabla ya wanaadamu na walikuwa wakifanya ufisadi mkubwa na Allaah akawaondoa na kuwaleta wanadamu." Maneno kama haya pia yalisemwa na Hassan Al-Basry (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na akaongeza kusema:

 

"Hii ndiyo maana Malaika wakamuuliza Rabb wao suali hilo."

 

Uhusiano Baina Ya Jinni Na Shaytwaan

 

Shaytwaan na Jinni asili yao ni moja, hapana hitilafu baina ya maulamaa kuhusu jambo hili, isipokuwa wamekhitalafiana katika suala; “Je Ibilisi ndiye baba wa Majinni (asili yao) mfano wa Adam ambaye ni baba yetu na asili yetu ?)”

 

Majibu:

Iblisi si asili yao, bali yeye ni miongoni mwao.

 

Allaah Anasema:

إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ

Isipokuwa Ibliys alikuwa miongoni mwa majini [Al-Kahf: 50]

 

Kwa vile Allaah Amemtaja Iblisi kuwa ni MIONGONI mwa majini, kwa hivyo yeye ni mmoja wao na si asili yao kama mfano wa Adam ('Alayhis-salaam) alivyokuwa asili ya wanadamu.

 

Tulisema kuwa wameitwa 'Majinni ' kwa sababu ya kutokuonekana kwao na sisi tumeitwa 'Insaan' kwa sababu ya kusahau kwetu, kwani neno 'Insan', asili yake linatokana na neno 'Nisiyaan', na maana yake ni Kusahau.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: "Adam alisahau na vizazi vyake vikasahau."

 

Ama neno 'Shaytwaan', katika lugha ya kiarabu maana yake ni 'Kila anayeasi na kupinga au kuzuwia au kushawishi viumbe wasiifuate njia ya Allaah', awe Jinni au Mwanadamu.

 

Allaah Anasema:

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا شَيَاطِينَ الْإِنسِ وَالْجِنِّ يُوحِي بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ زُخْرُفَ الْقَوْلِ غُرُورًا ۚ وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ مَا فَعَلُوهُ ۖ فَذَرْهُمْ وَمَا يَفْتَرُونَ ﴿١١٢﴾

Na hivyo ndivyo Tulivyojaalia kwa kila Nabiy maadui - mashaytwaan katika wana Aadam na majini wakidokezana wenyewe kwa wenyewe maneno ya kupambapamba na ya ghururi. Na lau Angetaka Rabb wako wasingeliyafanya hayo. Basi waachilie mbali na wanayoyatunga. [Al-An’aam: 112]

 

Iblisi Ni Katika Malaika?

 

Iblisi si katika Malaika, bali ni miongoni mwa Majinni kutokana na dalili zifuatazo:

 

Anasema:

 فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ

Wakasujudu isipokuwa Ibliys alikuwa miongoni mwa majini.. [Al-Kahf: 50]

 

Na Akasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ﴿٦﴾

Hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa. [At-Tahrym:  6] 

 

Kutokana na aya hii, tunapata ushahidi mwingine kuwa; Malaika hawamuasi Allaah. Kwa hivyo Ibilisi angelikuwa Malaika, asingemuasi Rabb wake bali angetenda kama alivyoamrishwa. Lakini yeye alitenda kinyume na hivo. Alimuasi Allaah pale alipokataa kumsujudia baba yetu Aadam ('Alayhis Salaam), akasema:

قَالَ مَا مَنَعَكَ أَلَّا تَسْجُدَ إِذْ أَمَرْتُكَ ۖ قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ ﴿١٢﴾

(Allaah) Akasema: Nini kilichokuzuia usisujudu Nilipokuamrisha? (Ibliys) Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, na yeye Umemuumba kwa udongo. [Al-A’raaf: 12]

 

Na hapa pia tunapata ushahidi mwingi pia kuwa Iblisi si miongoni mwa Malaika, kwani Malaika wameumbwa kwa Nuru na Mashaytwaan wameumbwa kwa moto.

 

Katika aayah iliyotangulia Iblisi alisema:

أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ

Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto…[Al-A’raaf: 12]

 

Angelikuwa yeye ni miongoni mwa Malaika angelisema;

 

“Mimi ni bora kuliko yeye umeniumba kwa Nuru".

 

Kwa sababu Malaika wameumbwa kwa Nuru kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika hadiyth iliyotangulia:

 

"Malaika wameumbwa kwa nuru na Majini kwa ndimi za moto na Adam (ameumbwa) kwa mliyokwisha elezewa (Udongo)." [Muslim na Ahmad bin Hanbal]

 

Aina Za Majini

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

"Majini (wako) namna tatu, namna moja wana mabawa wanaruka na namna (nyengine) majoka na n’ge na namna nyengine hawaishi mahala pamoja na hupenda kuhama." [Atw-Twabaraaniy na Al-Haakim na Al-Bayhaqiy na imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy]

 

Mahali Wanapoishi

 

Majini wanaishi katika majangwa na katika sehemu za kutupa taka, kwa sababu wao wanakula mabaki ya vyakula vya binadamu.

 

Zimepokelewa hadiyth nyingi pia kwa njia ya Ibni 'Abbaas na Ibni Masaood (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akienda jangwani na kuwasemesha Majinni na kuwalingania katika dini ya Kiislamu na kuwataka wamuabudu Allaah mmoja wa kweli.

 

Majinni wanapenda pia kuishi vyooni, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ametufundisha dua ya kusoma kabla ya mtu kuigia chooni, akasema:

 

Mmoja wenu anapoingia chooni basi aseme:

 

"Allaahumma inniy audhu bika minal khubuthi wal khabaaith."

 

Na maana yake:

 

“Allaah najikinga kwako kutokana na majini wanaume na majini wanawake.” [Al-Bukhaariy na Muslim.]

 

Majini pia wanaishi katika Mashimo:

 

Kutoka kwa Qataadah kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

"Mmoja wenu asikojowe ndani ya shimo."

Na alipoiulizwa kuna ubaya gani mtu kukojoa ndani ya shimo akasema:

"Inasemekana kuwa Majinni wanapenda kuishi humo."

[Annasaiy]

 

Wanakula Na Kunywa

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

"Mmoja wenu anapokula, basi ale kwa (mkono wa) kulia na anapokunywa anywe kwa (mkono wa) kulia, kwa sababu Shaytwaan anakula kwa kushoto na kunywa kwa kushoto." [Muslim]

 

Na akasema:

 

"Mtu anapoingia nyumbani akasema; 'BismiAllaah', na anapokula (akasema BismiAllaah), Shaytwaan husema; 'Hatuna makazi humu (ndani ya nyumba hii), na hatuna chakula cha usiku'. Ama anapoingia asiseme; 'BismiAllaah', Shaytwaan husema; 'Tumepata makazi humu', na asiposema BismiAllaah pale anapokula, basi (Shaytwaan) husema; 'Tumepata makazi na chakula". [Muslim]

 

Wana Uwezo Wa Kujigeuza

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

“Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alinipa jukumu la kulinda (chakula cha) zaka ya Ramadhwaan, akaja mtu akawa anaiba katika chakula kile, nikamkamata na kumuambia kwamba nitampeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), akasema: 'Mimi ni muhitaji na nina watoto wengi na shida nyingi."

Anasema (Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

"Nikamuacha aende zake, na asubuhi yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaniuliza:

“Ee Abu Hurayrah umefanya nini na mfungwa wako jana?"

"Akasema:

 "Nikamwambia:

"Ee Rasuli wa Allaah, alinisikitikia shida zake na watoto wengi nikamuonea huruma nikamuacha."

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

“Ama huyu amekudanganya na atarudi.”

Nikajuwa kwamba atarudi kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema hivyo. Nikamtegea, akaja tena siku ya pili kuiba chakula, nikamkamata, nikamuambia nitakupeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Akaniambia:

“Mimi ni muhitaji na nina watoto wengi sitorudia tena.”

Nikamuacha aende zake, na asubuhi yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

“Ee Abu Hurayrah umefanya nini na mfungwa wako jana?”

Nikamuambia:

"Ee Rasuli wa Allaah, alinisikitikia shida zake na watoto wengi nikamuonea huruma nikamuacha."

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

 "Ama huyu amekudanganya na atarudi."

Nikamkamata mara ya tatu akiwa anaiba (tena) chakula, nikamuambia:

"Nitakupeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na hii ni mara ya tatu na kila mara unasema hutorudia kisha unarudia."

Akasema:

"Niache nikufundishe maneno Allaah atakufaa nayo."

Nikamuuliza;

“Maneno gani hayo?"

Akasema:

“Unapokuwa juu ya tandilo lako soma Ayatul Kursy - Allaahu laa ilaaha illa huwal hayyul qayuum - mpaka mwisho na itaendelea kukuhifadhi aya hii na hatokukaribia Shaytwaan mpaka utakapoamka.”

Nikamuacha aende zake.

Asubuhi yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaniuliza:

“Amefanyaje mfungwa wako jana?”

Nikamuambia:

"Ee Rasuli wa Allaah amejidai eti amenifundisha maneno ambayo Allaah Atanifaa nayo, basi nikamuacha huru."

Akaniuliza;

“Ni maneno gani hayo?”

Nikasema:

"Ameniambia:

“Unapokuwa juu ya tandiko lako soma Ayatul Kursy mpaka mwisho na Allaah ataendelea kukuhifadhi nayo na hatokukaribia Shaytwaan mpaka utakapoamka."

 Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

"Ama yeye amesema kweli ingawaje ni muongo. Unamjua nani uliyekuwa ukizungumza naye siku tatu hizi ewe Aba Hurayrah?"

Nikajibu:

"La simjuwi".

Akasema:

“Yule ni Shaytwaan.”

[Al-Bukhaariy]

 

Kwa vile Shaytwaan huyu aliyekuwa akiiba alikuwa akimjia Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwa sura ya binadamu, basi hii ni dalili kwamba majini wanao uwezo wa kujibadilisha umbile lao.

 

Wamo Miongoni Mwao Wanawake Na Wanaume

 

Katika hadiyth niliyoitaja hapo juu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema:

 

"Anapoingia mmoja wenu chooni, basi aseme: “Allaah najikinga kwako kutokana na majini wanaume na majini wanawake” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Wanaowa?

 

Majini wanaoana na kuzaliana, na ushahidi umo ndani Qur-aan katika kauli Yake Subhaanahu wa Ta’aalaa Aliposema:

ۗ أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ ۚ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلًا ﴿٥٠﴾

Je, basi mnamfanya yeye na kizazi chake walinzi pasi Nami; na hali wao kwenu ni maadui? Ubaya ulioje mbadala huu kwa madhalimu.   [Al Kahf: 50]

 

Hata hivyo ‘Ulamaa wengi hawakubali majini waowane na wanadamu. Pana kisa cha mwanamke mmoja kutoka Yemen alikuwa akidai kwamba anajiwa na jinni na kwamba jinni huyo anataka kumuowa. Alipoulizwa Imam Malik kuhusu jambo hili akasema:

 

“Sioni kifungu chochote cha sheria kinachoharamisha, isipokuwa nakuogopeeni fitna (Mitihani).”

 

‘Ulamaa wamesema kuwa kauli ya Imam Malik hii inatujulisha juu ya hofu yake, kwani mwanamke yeyote anaweza kujipatia mimba kwa njia zisizo za halali, kisha akasema kwamba ameolewa na jinni na kwa njia hii uhuni utazidi na fitna zitaenea.

 

‘Ulamaa wengine wamekataa kabisa fikra ya kuoana baina ya majini na wanadamu wakiegemea kauli ya Allaah Isemayo:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ 

Na katika Aayaat (ishara, dalili) Zake ni kwamba Amekuumbieni katika jinsi yenu wake ili mpate utulivu kwao; [Ar-Ruwm: 21]

 

Na Akasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَجَعَلَ لَكُم مِّنْ أَزْوَاجِكُم بَنِينَ وَحَفَدَةً

Na Allaah Amekufanyieni wake katika jinsi yenu; na Amekufanyieni katika wake zenu wana na wajukuu…; [An-Nahl: 72]

 

Katika aayah hizi Allaah anatufahamisha kwamba ametuumbia wake zetu katika jinsi yetu, wakati Majinni si katika Jinsi yetu. Na akasema; Ili mupate utulivu kwao", wakati mwanadamu hawezi kupata utulivu kwa jinni, maana siku zote mtu hupata utulivu kwa kiumbe aliye mfano wake na majini si mfano wetu.

 

Majini Wanakufa?

 

Allaah Anasema:

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ ﴿٢٦﴾

Kila aliyekuwa juu yake (ardhi) ni mwenye kutoweka. [Ar-Rahmaan: 26]

 

Na Akasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَلَا تَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ ۘ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ ۚ 

Na wala usiombe pamoja na Allaah mwabudiwa mwingine. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. [Al-Qaswas: 88]

 

Inavyojulikana ni kwamba Iblisi yuhai mpaka siku ya Qiyaamah.

 

Allaah Amesema:

قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ﴿٣٦﴾قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ﴿٣٧﴾إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ﴿٣٨﴾

Akasema: Rabb wangu! Nipe muhula mpaka Siku watakayofufuliwa. (Allaah) Akasema: Basi hakika wewe ni miongoni mwa waliopewa muhula. Mpaka siku ya wakati maalumu. [Al-Hijr: 36-38]

 

Kwa hivyo Ibilisi ataishi mpaka siku maalum anayoijua Allaah peke yake kisha atakufa, na majini nao pia wanazaliana na wanakufa kama sisi.

 

Wamo Miongoni Mwao Waislam Na Makafiri

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amesema:

وَأَنَّا مِنَّا الْمُسْلِمُونَ وَمِنَّا الْقَاسِطُونَ ۖ فَمَنْ أَسْلَمَ فَأُولَـٰئِكَ تَحَرَّوْا رَشَدًا﴿١٤﴾

Na kwamba miongoni mwetu ni Waislamu, na miongoni mwetu wakengeukaji haki; hivyo atakayesilimu, hao ndio waliofuata uongofu. [Al-Jinn: 14]

 

Na Akasema:

وَأَنَّا مِنَّا الصَّالِحُونَ وَمِنَّا دُونَ ذَٰلِكَ ۖ كُنَّا طَرَائِقَ قِدَدًا﴿١١﴾

Na kwamba miongoni mwetu ni wema, na miongoni mwetu kinyume chake; tumekuwa makundi ya njia mbali mbali. [Al-Jinn: 11]

 

Katika kuifasiri aayah hii, anasema Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

"Kauli ya Allaah; “Tumekuwa njia mbali mbali”, maana yake ni “Makafiri na Waislamu”.

 

Baadhi ya ‘ulamaa wanasema:

 

"Dini mbali mbali na madhehebu mbali mbali."

 

Waislamu Katika Majini Wataingia Jannah? 

 

Katika tafsiri yake Ibni Kathyir amesema:

 

"Waislamu miongoni mwa Majini wataingia Jannah kama Waislamu katika wanadamu "Na dalili yake pamoja na dalili za maulamaa wengine ni kauli ya Allaah akitujulisha juu ya hali ya wanawake wa Jannah Aliposema:

لَمْ يَطْمِثْهُنَّ إِنسٌ قَبْلَهُمْ وَلَا جَانٌّ ﴿٧٤﴾

Hajawabikiri binadamu kabla yao wala jini. [Ar-Rahmaan: 74]

 

Na Aliposema:

وَلِمَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ جَنَّتَانِ ﴿٤٦﴾فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٤٧﴾

Na kwa mwenye kukhofu kisimamo mbele ya Rabb wake atapata bustani mbili. Basi ni zipi neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?  [Ar-Rahmaan: 46-47]

 

Allaah Amejaalia jazaa ya majini na binadamu wema kuwa ni jannah, na majini waliijibu aya hii kwa kumshukuru Allaah wakasema:

 

"Hapana katika neema zako zozote zile tunazozikanusha kwa hivyo shukrani zote ni Zako."

 

Hii ni hadiyth iliyosimuliwa na Imam At-Tirmidhiy kutoka kwa Jabir (Radhwiya Allaahu anhu) kwamba amesema:

 

"Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliisoma Suwrah Rahman mpaka mwisho kisha akasema: ‘Mbona mumenyamaza kimya, Majini wamekuwa bora kuliko nyinyi kwa kujibu kila ninapowasomea aayah hii:

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٤٩﴾

Basi ni zipi neema za Rabb wenu mnazikadhibisha? [Ar-Rahmaan: 49]

 

Wao huijibu kwa kusema:

 

"Hapana katika neema zako zozote zile tunazozikanusha kwa hivyo shukrani zote ni Zako."

Imesimuliwa na At-Tirmidhiy na Al-Bazaar na Al-Haakim na pia Ibni Jariyr na Shaykh Al-Albaaniy amesema kwamba hadithi hii ni njema.

 

Dalili inayopatikana kutoka katika aayah hizi ni kwamba; Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiwapa Majini mafundisho ya Dini, na kuwafahamisha kwamba pana jaza ya Jannah kwa Mwenye kuogopa.

 

Kama Majini hawatoingia Jannah hapangekuwa na haja ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwatokea na kuwapa mafunzo ya dini na kuwajulisha juu ya Jannah inayowangoja wale wanaomuogopa Allaah.

 

Majini Wanawaogopa Wanadamu

 

Ameeleze Ibn Abi Al Dunya kwamba Mujahid amesema:

 

‘Usiku mmoja nilikuwa nikiswali akanitokea mfano wa mtoto mdogo mbele yangu nikamshika kwa nguvu zangu zote akainuka na kuuruka ukuta hata nilisikia kishindo cha kuanguka kwake.’  Akaendela kusema: ‘Wao (majini) wanakuogopeni kama nyinyi mnavyowaogopa."

 

Imepokelewa kutoka kwa Mujahid kuwa alisema:

 

‘Shaytwaan anakuogopeni kuliko nyinyi mnavyomuogopa akikukaribia usimregezee akakupanda, bali shindana naye na hatimae ataondoka."

 

Kuweza Kwa Majini Kusikia Habari Za Mbinguni

 

Imepokelewa kutoka kwa Ibni 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba alisema:

 

‘Amenihadithia mmoja katika Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa, usiku mmoja walipokuwa wamekaa pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) nyota moja ikaanguka na kun’gara. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akawauliza:

"Mlikuwa mkisemaje wakati wa ujahilia (kabla ya kuja Uislamu?"

Wakajibu:

 

"Tulikuwa tukisema; Usiku wa leo amezaliwa mtu mtukufu na amekufa mtu mtukufu."

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akawaambia:

 

"Bali haiangushwi nyota kwa ajili ya kifo cha mtu wala kwa kuzaliwa kwa mtu, lakini Rabb wetu Aliyetukuka anapotoa amri, Malaika wabebao Arshi husabbih (husema Subhana Allaah), na viumbe vya mbinguni vyote humsabihi Allaah pia, kisha husabihi viumbe wa mbingu za chini mpaka habari inapofika katika mbingu ya dunia, majini huzipata habari hizo na huwatupia mabwana zao nazo ni habari za kweli, lakini wao huongeza habari za uongo juu yake.”

 

Kutokana na Bibi 'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa), amesema:

"Niliuliza:

"Ee Rasuli wa Allaah, makuhani walikuwa wakituelezea baadhi ya mambo na yalikuwa ni ya kweli."

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

"Hiyo ni habari ya kweli ameipokea jini akamtupia bwana wake na kuongezea uongo mara Mia."

[Imetolewa na Maimaam Al-Bukhaariy na Muslim na Ahmad na AlBayhaqiy]

  

NA  ALLAAH ANAJUA  ZAIDI

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Eda: Maana ya Eda, Hikma ya Eda , Hukmu zake, Mambo yanayopasa na uyasiyopasa kwa mwenye Eda

Namna ya Kuswali Swalat Kusuwf (Swalah ya Kupatwa kwa Jua/Mwezi

Ramadhwaan ni Mwezi wa Du’aa na Du’aa hutakabaliwa