Kuinunua na Kuisafirisha Zakaah

 KUINUNUA NA KUISAFIRISHA ZAKAAH


Mtume Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amekataza mtu kuinunua Zakaah yake. 


Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Llaahu ‘anhu), amesema:

 

"‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimtoa farasi wake Swadaqah fiy sabiyli Llaah, kisha akamkuta farasi huyo anauzwa na akataka kumnunua. Akamuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya jambo hilo, akamwambia:

 

"Usimnunue na wala usirudie (kutaka kuimiliki tena) Swadaqah yako" [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

 

Baadhi ya maulamaa wakasema kuwa kukataza huko ni kwa ajili ya kujiepusha tu, na si kwa ajili ya kuharamisha, wakiegemea Hadiythi nyingine inayoruhusu mtu kuipokea Swadaqah yake kama zawadi itokayo kwa masikini aliyempa.



Hukmu  ya Kuisafirisha Zakaah



‘Ulamaa wengi wamekubali kuwa mali ya Zakaah (Zakaatul Maal - si Zakaatul Fitwr) inaweza kusafirishwa na kutolewa katika nchi nyingine kwa wanaoistahiki zaidi ikiwa watu wa mji anaoishi mtoaji hawaihitajii zaidi mali hiyo. Ama ikiwa katika nchi hiyo wapo wanaoihitajia, basi zipo Hadiyth zinazotujulisha kuwa Zakaah ya kila nchi wanapewa masikini wake.

 

Katika madhehebu ya Imaam Abu Haniyfah, wao wanasema:

 

"Ni Makruuh kuisafirisha mali ya Zakaah isipokuwa ikiwa kwa ajili ya kumsaidia ndugu wa nasaba mwenye kuihitajia, na hii inatokana na umuhimu wa kuunganisha undugu huo, au pia kwa ajili ya watu wenye shida sana katika watu wa nchi yake, au kwa ajili ya kuiondoa kutoka nchi ya kikafiri na kuipeleka katika nchi ya kiislam."

 

Madhehebu ya Imaam Ash-Shaafi’iy yanasema:

 

"Haijuzu kuisafirisha mali ya Zakaah na inawajibika kutolewa katika nchi iliyochumwa mali hiyo isipokuwa pakikosekana wenye kuihitajia Zakaah hiyo katika nchi hiyo".

 

Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipewa ugavana wa nchi ya Yemen na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na alipotawala ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimuacha Mu’aadh aendelea kuwa gavana wa nchi hiyo. Lakini Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipompelekea ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) theluthi ya mali ya Zakaah, ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikataa kuzipokea akamwambia:

 

"Sikukupeleka uwe mchotaji (wa mali) wala mpokeaji wa kodi, bali nimekupeleka kwa ajili ya kuchukua mali (ya Zakaah) kutoka kwa matajiri wao na kuzirudisha kwa masikini wao".

 

Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

 

"Nisingekuletea ila kwa sababu sikumpata (masikini) anayezistahiki kuzichukua".


Hukmu ya Kuidhihirisha Zakaah



 

Inazuju kwa mtoaji kuidhihirisha au kuitoa kwa siri Zakaah yake, yote sawa ikiwa anachokitowa ni Swadaqah ya kawaida au Zakaah ya mali, ingawaje kuitoa kwa siri ni bora zaidi.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

إِن تُبْدُواْ الصَّدَقَاتِ فَنِعِمَّا هِيَ وَإِن تُخْفُوهَا وَتُؤْتُوهَا الْفُقَرَاء فَهُوَ خَيْرٌ لُّكُمْ

Mkidhihirisha swadaqah basi ni vizuri hivyo, na mkizificha na kuwapa mafakiri, basi hilo ni khayr kwenu. [Al-Baqarah: 271]

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Watu saba Allaah  Atawafunika katika kivuli Chake, Siku ambayo hakutokuwa na kivuli ila kivuli Chake: Imaam muadilifu, kijana ambaye amekulia katika ‘Ibaadah ya Rabb wake, Mtu ambaye moyo wake umeambatana na Misikiti, watu wawili wanaopendana kwa ajili ya Allaah; wanakutana kwa ajili Yake na wanafarikiana kwa ajili Yake, mwanamme aliyetakwa na mwanamke mwenye hadhi na mrembo wa kuvutia akasema: "Mimi namkhofu Allaah!" Mtu aliyetoa Swadaqah yake akaificha hadi kwamba mkono wake kushoto usijue nini ulichotoa mkono wa kulia, na mtu aliyemdhukuru Allaah kwa siri macho yake yakatokwa machozi." [Al-Bukhaariy - Muslim na Imaam Ahmad]

MWISHO

Na Allaah anajua zaidi 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Eda: Maana ya Eda, Hikma ya Eda , Hukmu zake, Mambo yanayopasa na uyasiyopasa kwa mwenye Eda

Namna ya Kuswali Swalat Kusuwf (Swalah ya Kupatwa kwa Jua/Mwezi

Ramadhwaan ni Mwezi wa Du’aa na Du’aa hutakabaliwa