Kufaradhishwa kwa Zakaah na Umuhimu wake
KUFARADHISHWA KWA ZAKAAH NA UMUHIMU WAKE
KUFARADHISHWA KWA ZAKAAH
Zakaah imefaradhishwa wakati Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa Makkah katika siku za mwanzo za Uislaam, lakini hapakuwekwa Nisaab, (kiwango cha mali ambacho mtu akiwa nacho kwa muda wa mwaka analazimika kuitolea Zakaah), wala kiasi cha kulipa, isipokuwa waliachiwa Waislam wenyewe kukisia kiasi cha kutoa.
Katika mwaka wa Pili baada ya Hijrah, ilifaradhishwa kiasi chake katika kila aina ya mali na kubainishwa vizuri.
UMUHIMU WA ZAKAAH KATIKA QUR-AAN
Katika Qur-aan tukufu na katika Mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), yamo mafunzo mengi yanayopendekeza Kutoa Zakaah na yanayowakemea wale wasioitoa.
Katika Qur-aan Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا
Chukua (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo. [At-Tawbah: 103]
Na maana yake ni "Chukua ee Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Swadaqah maalum kutoka katika mali za Waislam na uwape wanaostahiki ili wenye mali 'wasafike' kutokana na uchafu wa ubakhili na tamaa, na kutokana na ubaya wa kuwanyima masikini haki zao na pia 'uwatakase' nafsi zao kwa Swadaqah hizo na wapate baraka za Rabb wao ili waweze kupata furaha za hapa duniani na za huko Aakhirah.
Na Akasema:
إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ. آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَلِكَ مُحْسِنِينَ. كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ. وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ. وَفِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ
Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu. Wakichukua yale Atakayowapa Rabb wao. Hakika wao walikuwa kabla ya hapo ni wahisani. Walikuwa kidogo tu katika usiku wakilala kwa raha. Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfirah. Na katika mali zao kuna haki maalumu kwa mwenye kuomba na asiyeomba. [Adh-Dhaariyaat: 15-19]
Katika Aayah hii Allaah Anatuelezea juu ya wale atakaowaingiza katika bustani Zake na chemchem, kwa sababu walipokuwa huko duniani walikuwa wenye kulala muda mfupi sana nyakati za usiku, na sehemu kubwa ya usiku, walikuwa wakiswali, na nyakati za kabla ya kuingia alfajiri walikuwa wakiomba maghfira huku wakijikurubisha kwake Subhanaahu wa Ta’aalaa.
Walikuwa pia watu wenye kutoa katika mali zao kuwapa fakiri na maskini, wenye kuomba na wasiyo omba huku wakiwaonea huruma.
Na Allaah Akasema pia:
وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاء بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلاَةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللّهَ وَرَسُولَهُ أُوْلَـئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللّهُ إِنَّ اللّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ
"Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wandani wao kwa wao, wanaamrisha mema na wanakataza munkari na wanasimamisha Swalaah na wanatoa Zakaah na wanamtii Allaah na Rasuli Wake. Hao Allaah Atawarehemu. Hakika Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote". [At-Tawbah - 71]
UMUHIMU WA ZAKAAH KATIKA HADIYTHI (SUNNAH)
Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Mambo matatu naapa juu yake na nakuhadithieni Hadiyth muihifadhi (vizuri).
Mali haipungui kwa kutoka Swadaqah, na mtu anapodhulumiwa akasubiri, basi Allaah humuongezea utukufu, na mtu anapojifungulia mlango wa kuombaomba, basi Allaah humfungulia mlango wa ufakiri". [At-Tirmidhiy kutoka kwa Abuu Kabshah Al-Anmaary (Radhwiya Allaahu ‘anhum)]
Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa; Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Hakika Allaah anazikubali Swadaqah na anazipokea kwa mkono wake wa kuume na anailea kama mmoja wenu anavyomlea nyumbu wake mpaka tonge (anayoitoa Swadaqah) inafikia ukubwa wa jabali Uhud". [Ahmad - At-Tirmidhiy na ameisahihisha]
Hadiythi hii inatujulisha kuwa mtu anapotoa Zakaah au Swadaqah, basi Zakaah hiyo inaingia mikononi mwa Allaah Subhanaahu wa Ta’aalaa kwanza, kabla haijaingia mikononi mwa masikini anayepewa, ikitufahamisha jinsi gani Allaah anavyoitukuza ‘Ibaadah hii ya Kutoa Zakaah na jinsi anavyompenda mja wake mwenye kutoa Zakaah au Swadaqah hata akaipokea kwa mikono yake Mwenyewe Subhanaahu wa Ta’aalaa kwanza, akaizidisha jaza yake na kuifanya iwe na ukubwa wa Jabali Uhud.
Anasema Waki’iy:
"Hadiyth hii pia inasadikisha kauli yake Subhanaahu wa Ta’ala katika Qur-aan pale Aliposema:
أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ هُوَ يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَأْخُذُ الصَّدَقَاتِ
Je, hawajui kwamba Allaah Ndiye Anayepokea tawbah ya waja Wake, na Anapokea Swadaqah. [At-Tawbah: 104]
Na Aliposema:
يَمْحَقُ اللَّـهُ الرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ ۗ
Allaah Huifuta baraka (mali ya) ribaa na Huzibariki swadaqah.[Al-Baqarah - 276]
Imepokelewa kuwa Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
"Mtu mmoja kutoka katika kabila la Bani Tamiym alimwendea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia:
"Ee Rasuli wa Allaah, mimi nina mali nyingi na nina jamaa wengi na wageni huja kwangu kwa wingi. Kwa hivyo nijulishe nini nifanye na vipi nitowe?"
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
"Utoe Zakaah kutoka katika mali yako, kwa sababu hiyo ni tohara itakayokutahirisha, na uwaendee watu wako (ndugu zako wa nasaba), na uijue haki ya masikini na ya jirani na ya muombaji". [Ahmad]
Na Kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Mambo matatu naapa juu yake, Allaah hawezi kumfanya aliye na sehemu yake katika Uislam akawa sawa na yule asiye na sehemu. Na sehemu za Uislaam ni tatu. Swalaah, Funga na Zakaah. Na Allaah Anapokuwa pamoja na mja wake hapa duniani, basi huko akhera hamuachi akawa na mwengine asiyekuwa Yeye. Na mtu anayewapenda watu hapa duniani, basi siku ya Qiyaamah Allaah Atamjaalie awe pamoja nao…" [Ahmad]
Na kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
"Mtu mmoja alimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam);
"Ee Rasuli wa Allaah; Unasemaje juu ya mtu anayetoa Zakaah ya mali yake?"
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
"Atakayetoa Zakaah ya mali yake, keshaiondoa shari yake".
NA ALLAAH ANAJUA ZAIDI
Maoni
Chapisha Maoni